Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa msimamo wa kutumia haki ya kujilinda kiasili chini ya Sheria ya Kimataifa na kusisitiza kwamba haifanyi kazi ya kuongeza au kusambaza mgogoro, huku ikionya kuhusu machafuko zaidi ya kijeshi, yanayoweza kusababishwa na utawala wa Israeli.
![]() |
Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei |
Hayo yamebainishwa katika taarifa ilitolewa jana kwa vyombo vya habari na Serikali ya Iran kupitia Mtaalamu wa Ushauri wa Kitamaduni wa Ubalozi wa Iran nchini,Maulid Sengi.
"Tunatoa msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuhusu kutumia haki yake ya kujilinda kiasili chini ya Sheria ya Kimataifa, kujibu mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Israeli, dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran huko Syria," amesema Sengi na kuongeza;
"Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inarudia msimamo wake thabiti kwamba, haifanyi kazi ya kuongeza au kusambaza mgogoro katika eneo, inaonya kuhusu machafuko zaidi ya kijeshi yanayoweza kusababishwa na utawala wa Israeli."
Akifafanua zaidi Sengi amesema: " Iran inathibitisha tena azma yake isiyo na shaka ya kulinda watu wake, usalama wa kitaifa na maslahi, uhuru na utegemezi wa eneo dhidi ya tishio lolote au vitendo vya uvamizi na kujibu vitisho au uvamizi huo kwa nguvu na kulingana na sheria ya kimataifa."
Amebainisha kwamba Iran haina nia ya kushiriki katika mzozo na Marekani kwenye eneo hilo, lakini ikiwa Marekani itaanzisha operesheni za kijeshi dhidi ya Iran, raia wake au maslahi yake, Iran itaendelea kutunza haki yake ya asili ya kujibu kwa kipimo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Iran, kulikuwa na mazungumzo ya simu kati ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Aprili 2 na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hussein Amirabdollahian, ambayo yalijadili hali hiyo na kutaka hatua sahihi zichukuliwe, ikiwamo jumuia ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulaani uhalifu huo wa kutisha.
"Katika barua zetu zilizotumwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu (S/2024/281-5/2024/305), tumesisitiza kuwa shambulio la kigaidi la Israeli dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran huko Damascus, lilikuwa ukiukaji dhahiri wa sheria ya kimataifa ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, hasa Ibara ya 2 (4) ya Mkataba na uhuru, uhuru na utegemezi wa kieneo wa Jamhuri ya Arabuni ya Syria;
Hatua hiyo isiyo halali, inawakilisha uvunjaji wa kanuni na misingi iliyokubaliwa ulimwenguni ya kutotaka kushambuliwa kwa wawakilishi, majengo ya kidiplomasia na konsulari, ambazo ndiyo msingi wa uhusiano wa kimataifa,"amesema Sengi.
Amesema Iran ililitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukemea vikali kitendo cha jinai dhidi yake na kuchukua hatua thabiti za kuwafikisha mbele ya sheria watekelezaji wa shambulio hilo haraka na kuzuia kurudiwa kwa uhalifu wa aina hiyo dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya mwanachama yeyote wa Umoja wa Mataifa.
"Kama mwanachama anayehusika wa Umoja wa Mataifa, Iran inajitolea kwa madhumuni na kanuni zilizoorodheshwa katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa na inathibitisha kujitolea kwake katika kutaka kudumisha amani na usalama wa kimataifa;
"Ni wazi kwa wote kwamba vitendo visivyo na utulivu, vya kutokuwajibika vya Israeli dhidi ya mataifa katika eneo hilo la Mashariki ya Kati, hasa mauaji dhidi ya watu katika Gaza ni tishio halisi kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa,"imesema taarifa hiyo ya Iran.
April 13 mwaka huu vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilifanya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Israeli kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.
Hatua hiyo inadaiwa kichukuliwa na Iran kwa ilichoeleza kutumia haki ya kujilinda kiasili kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 51 ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, lakini pia kujibu mashambulizi ya kijeshi ya mara kwa mara ya Israeli, hasa la Aprili mosi, dhidi ya majengo ya kidiplomasia ya Iran, kinyume cha Ibara yla 2 (4) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Iran imesema hatua hiyo ilikuwa ni muhimu na sawa na ukubwa wake, ililenga malengo ya kijeshi, ilifanyika kwa umakini na uangalifu ili kupunguza uwezekano wa kuzuka kwa mgogoro na kuzuia madhara kwa raia.
Katika taarifa yake, Iran imesema imelijulisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya vitendo haramu vya kimataifa vya Israeli pamoja na haki ya asili ya Iran, chini ya sheria ya kimataifa ya kujibu mashambulizi ya kigaidi kama hayo.
0 Maoni