Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), BengI Issa, amewataka wanawake na vijana kutumia vizuri na kwa nidhamu fedha zinazotolewa na taasisi za uwezeshaji, ili kasi ya kujikwamua kiuchumi iongezeke na kuleta matokeo chanya kwa fedha zinazopelekwa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Wanawake na Vijana wa Kanisa la TAG City Light Temple, Goba, Dar es Salaam, Issa amesema Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan ina nia nzuri na wazi ya kuwawezesha Watanzania kiuchumi kwa kutoa mitaji wezeshi, hasa kwa makundi maalumu kwa kutumia majukwa ya uwezeshaji.
Amesema kasi ya kujikwamua kiuchumi itaongezeka na kuwa na matokeo chanya iwapo wawezeshwaji watatumia vizuri na kwa nidhamu fedha na raslimali zingine wanazopewa kupitia majukwaa wezeshi katika maeneo yao.
"Ni matumaini yangu wanawake na vijana wa Goba mtalitumia vizuri jukwaa hili kujiimarisha kiuchumi kwa kupata mikopo nafuu itakayokuza biashara zenu kwa kufanya shughuli zenye tija," amesema Issa.
Ameeleza kuwa uzoefu wa baraza unaonyesha kuwa wanawake wanakimbilia mikopo wanayoichukulia kuwa ni rahisi kuipata pasipokujua kuwa riba ni kubwa na itawakwaza katika marejesho.
"Tumegundua baadhi ya mikopo riba yake ni mara sita ya kiasi kilichochukuliwa. Wengine wanaingia mikataba ambayo hawakuisoma kabisa. Mwenendo huu unawaingiza wakopaji katika hasara kubwa na kurudi tena katika dimbwi la umaskini," ameeleza.
Katika risala yake, jukwaa hilo limeeleza kuwa linatarajia mipango yake kugharimu Sh. 131 milioni ambapo Kanisa limetoa matofali 300 kujenga Shule ya Msingi ya Matosa; limetoa riflekta 100 kwa madreva wa bodaboda, huku waumini wakitoa damu salama na jana kanisa lilitoa taulo za kike zenye thamani yaSh. 320,000.
Katika hotuba yake, Mchungaji Kiongozi wa kanisa la hilo, Dk Omar Mulenda, ameshauri watoto wahimizwe kuthamini elimu na wasome bila kukatisha masomo.
"Tusikubali mtoto kukaa nyumbani bila kwenda shuleni; tuwalee katika maadili mazuri na wazazi na jamii tusipuuze mahitaji ya watoto, bali watimiziwe," amesema.
Naye Mjasiriamali Bahati Daudi, amesema Serikali imejitahidi kuwajengea uwezo wanawake na vijana na wengi wao kujiajiri kupitia vikundi vyao wamepata mikopo yenye riba nafuu na kukuza mtaji yao na kukuza uchumi stahimilivu wa familia.
NEEC imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha maona na matarajio ya serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia ya kuhakikisha mifuko wezeshi inatoa mchango stahiki ikiwemo utoaji wa mitaji wezeshi kwa makundi maalumu.
Mwisho
0 Maoni