-Yatakuwa kwenye ofisi zake
-Waziri aagiza mkurugenzi kusimamishwa kazi
-Ataka waliomilikishwa maeneo ya wazi kujisalimisha
-Ni katika siku 100 akiwa ofisini
Exuperius Kachenje, daimatz@gmail.com
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa amesema wizara hiyo itaanzisha maduka ya ardhi katika ofisi zake na wilaya na mikoa.
Amesema, lengo la hatua hiyo ni kukoa wananchi dhidi ya udanganyifu unaofanyika kwenye ununuzi wa ardhi maeneo mbalimbali kwa sasa.
Akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya Habari nchini kupitia, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), kuhusu siku 100 tangu alipoingia kuiongoa wizara hiyo Dar es Salaam leo Desemba 22, 2023 Waziri Silaa amebainisha hayo.
Waziri Silaa ametangaza kupiga marufuku mauziano holela ya ardhi ambazo hazijapangwa kuanzia sasa, akipiga marufuku pia wenyeviti wa mitaa kujihusisha na uuzaji ardhi.
![]() |
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa |
"Tunazo takwimu zinaonyesha kuna kampuni binafsi mbaya za upimaji, tutazitaja hadharani, lakini naelekeza kampuni zote za upimaji na uuzaji ardhi zenye uadilifu zifungue madawati katika ofisi za ardhi wilaya na mikoa, wizara itafungua maduka ya ardhi, hili Katibu Mkuu atalitolea maelekezo," amesema Waziri Silaa na kufafanua:
"Hapa natoa katazo, maeneo ambayo yameiva kimji, ya manispaa,miji na majiji, ni marufuku kuuza eneo ambalo halijapimwa; sasa maeneo yote yatapimwa na Serikali. Tangazo hili linawaondosha wenyeviti wote wa mitaa katika kuuza ardhi na kuchukua fedha za waanchi za mauzo ya ardhi. "
Badala yake Silaa amesema, maduka hayo ya ardhi yatakayokuwa kwenye ofisi za wizara yataratibiwa na wizara yake kutumia mtandao yakitoa nafasi pia kwa kampuni binafsi za upimaji na uuzaji ardhi zenye uadilifu, kufanya kazi hiyo bila kuhusisha fedha tasilimu bali kwa njia ya benki na njia za kielektoniki ili kuhakikisha fedha za wananchi hazipotei.
Huku akieleza dhamira ya wizara yake kupanga, kupima na kurasimisha ardhi ni kutokana na kasi ya ukuaji miji na makazi kuwa kubwa, hivyo wizara yake itahakikisha maeneo hayo yanafanyiwa maboresho.
Waziri Silaa amesema katika uboreshaji huo, wataajiri vijana wenye utaalam wa ardhi kila kata, ambao watasaidia katika upimaji na kuboresha mipango miji kwa maeneo husika ambapo baadae watakuwa mawakala wa uuzaji ardhi kwa mfumo wa Serikali.
Kwenye mkutano huo, Waziri wa Ardhi pia amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, kumwandikia barua ya kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi wa wizara hiyo, kwa kile kilichoelezwa kuhusika na idara hiyo ka kuandaa kanuni zinazotoa mwanya wa ujenzi holela wa vituo vya mafuta.
Aidha Waziri Silaa ametoa hadi Januari 23 mwaka 2024 kwa wote waliomilikishwa au kukodishwa maeneo ya wazi kujisalimisha ili kuona uhalali wa kuwepo maeneo hayo na haki itendeke.
Akiongea zaidi kuhusu mageuzi ndani ya wizara yake, Silaa amesema wanakusudia kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo wa utendaji katika Sekta ya Ardhi yakilenga kuboresha utendaji kazi katika utoaji huduma za sekta ya ardhi.
Ameitaja Programu ya Kupanga, Kupima, Kumilikisha ardhi (KKK) kwa kushirikisha sekta binafsi na mamlaka za upangaji kuwa moja ya maboresho hayo ambapo yatafanya marekebisho ya utaratibu wa kukopesha fedha kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Viwanja utakaokuwa unatunza fedha na kukopesha fedha kwa ajili ya KKK.
Kwa mujibu wa Silaa Wizara hiyo inakamilisha maboresho ya mfumo wa TEHAMA utakaoruhusu huduma na miamala ya sekta kuanza kutolewa kidigitali mfumo utakaoanza kutumika hivi karibuni kwa k mikoa ya Tanga, Arusha, Mbeya na Mwanza.
Katika mkutano huo Waziri Silaa pia amezindua rasmi mfumo wa ARDHI KLINIKI KIGANJANI ambao ni maalumu kwa kupokea na kushughulikia malalamiko yote yatakayowasilishwa kiurahisi kwa kutumia simu ya kiganjani au kompyuta kuwahudumia watanzania katika sekta ya ardhi.
Kwa mujibu wa Waziri Silaa mabadiliko ya kimuundo na ya kiutendaji yatafanyika wizarani humo kwa kuanzisha mikoa maalumu ya ardhi kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa.
"Kwa kuanzia tumeanza na mikoa ya Dodoma na Dar es Salaam, yanaweza kuendelea kufanyika katika mikoa yenye miamala mingi ya ardhi ikiwemo Mkoa wa Mwanza na Pwani," amesema Silaa.
0 Maoni