- Aanza panga pangua viongozi
- Agusa 24 wamo MaDc, Wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala
- Ateua, atengua, MaRC, Mawaziri joto lapanda
Mwandishi Wetu, daimatza@gmail.com
Siku, saa na dakika zinazidi kukatika kuelekea sikukuu ya Krismas inayoendana na kumalizika kwa mwaka 2023, ambayo huambatana na kutumiana salam za kutakiana heri na kupeana zawadi, ikiwa ni sehemu ya desturi ya maisha ya Watanzania.
Wakati sikukuu hizo zikisubiriwa, leo Desemba 14, 2023, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko yanayowagusa watendaji 24 katika ngazi ya mikoa, wilaya na halmashauri nchini.
Hatua hiyo ya Rais Dk. Samia inaweza kutafsiriwa kama 'ametanguliza zawadi' ya sikukuu kwa walioguswa, ikizingatiwa kwamba umefanyika siku 13 kabla ya kusherehekea Krisimas na siku 20, kabla ya kuhitimisha mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024, ikikumbukwa kwamba, 'zawadi ni zawadi'.
Taarifa ya Ikulu kupitia kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, leo Desemba 14,2023, imeeleza kuwa Rais Dk. Samia amefanya uteuzi na uhamisho wa viongozi hao ulioanzia Desemba 12, 2023, sanjari na kutengua uteuzi wa Veronica Vicent Sayore aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega.
Nafasi ya Sayore imechukuliwa na Michael Kachoma, aliyetangazwa na Ikulu leo kushika wadhifa huo.
Katika uteuzi, Rais Samia amemteua Maryam Ahmed Muhaji kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, akichukua nafasi ya Karoline Mthapula ambaye atapangiwa kazi nyingine. Kabla ya uteuzi huo, Muhaji alikuwa Mkurugenzi wa Wilaya ya Wanging'ombe.
Rais Samia, amemteua Zuhura Abdulrahman Rashid kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, akichukua nafasi ya Shamim Sadiq ambaye atapangiwa kazi nyingine. Kablya ya uteuzi huo, Zuhura alikuwa Ofisa Mwandamizikatika Mfuko wa Taifa wa Maji.
Sanjari na uteuzi huo, Rais Samia, 'amewachekecha' wakuu wa wilaya sita kwa kuwahamisha vituo vya kazi, huku pia akiwachekecha Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri 15 nchini kwa kuwapangia vituo vipya vya kazi.
Hatua hiyo ya Rais Samia, inadaiwa kuleta tumbo joto kwa wateule wengine katika ngazi hizo, sanjari na wakuu wa mikoa na mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Sita, wakibaki na maswali kama watakula Sikukuu ya Krismas wakiwa kwenye nafasi zao ama la.
Mbali ya kudaiwa kuleta tumbo, imekuja siku chache kabla ya kuingia mwaka 2024, ambao utashuhudia uchaguzi wa Serikali za mitaa kufanyika, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa madiwani, wabunge na Rais, mwaka 2025.
Soma uteuzi kamili hapa chini;
0 Maoni