Mwandishi Wetu,daimatz@gmail.com
Ikulu ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetangaza kuwa kinu cha kwanza cha kuzalisha umeme katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, kitawashwa Januari 2024, ikiwa ni takriban siku 14 kuanzia leo.
Tangazo hilo la Ikulu limekuja huku maeneo mbalimbali ya Tanzania yakikabiliwa na mgawo wa umeme, hali inayotajwa kiuchangia kushuka kwa uzalishaji.
Hata hivyo, Bwawa hilo la Mwalimu Nyerere linatarajiwa kumaliza tatizo la upungufu wa umeme nchini kwa kuzalisha megawat 2100, litakapokamilika.
Katika taarifa yake, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus leo Desemba 18,2024, amemnukuu Rais Samia akieleza;
" Serikali inatarajia kuwashwa kinu cha kwanza cha kufua umeme mwezi Januari, 2024 katika bwawa la Nyerere, ikiwa ni jitihada za kuzalisha umeme wa kutosha ambao ni muhimu kwa wazalishaji."
Rais ameeleza hayo katika hafla ya utoaji Tuzo za Rais kwa wazalishaji bora, (PMAYA) jijini Dar es Salaam, ambapo amewataka wazalishaji wa bidhaa kupitia Shirikisho la Wenye Viwanda nchini, (CTI), kuendelea kuimarisha ubora wa bidhaa wanazozalisha nchini.
Huku akieleza kuwa Sarikali imeimarisha miundombinu ya barabara na bandari ili bidhaa zinazozalishwa zisafirishwe nje na kuingia nchini ili sekta ya viwanda iendelee kufanya vizuri, Rais Samia amewataka wazalishaji hao kuongeza juhudi katika uzalishaji na uongezaji wa bidhaa ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Rais amesema, mbali na kukua kwa sekta ya utalii, jitihada nyingine inayofanywa na Serikali kudhibiti dola ni kujishughulisha na kilimo hasa cha muda mfupi, kinachozalisha mazao kwa haraka.
0 Maoni