Vatican,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea Vatican City, Makao Makuu ya Kanisa Katoliki duniani na kiongozi wa kanisa hilo, Papa Francis.
Majaliwa na ujumbe wake, waliokuwa wakishiriki kwenye Mkutano wa Jukwaa la Kimataifa la Chakula Duniani, Maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 78 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) pamoja na Maadhimisho ya Siku ya 43 ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023.
Mjini Vatican, Majaliwa na ujumbe alioongozana nao walitembelea Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican na kujionea Altare na Makaburi ya Mapapa wa Kanisa Katoliki.
Habari kutoka tovuti rasmi ya Vatican zinaeleza kuwa katika kanisa hilo, ndimo Baba Mtakatifu huongoza Ibada mbalimbali kwa kipindi cha mwaka mzima.
Waziri Mkuu Majaliwa amefanya ziara hiyo Jumatano Oktoba 18, 2023, ambapo alitembelea chini ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, mahali ambapo wamezikwa baadhi ya Mababa watakatifu. Akiwa eneo hilo, Waziri Mkuu aliguswa na mahali alipozikwa Mtakatifu Yohane wa XXIII, ikikumbukwa kuwa wakati wa mkesha wa Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) Desemba 9, mwaka1961, Baba Mtakatifu huyo alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanganyika ili uhuru wake uwawezeshe wananchi wake kuishi maisha mema zaidi kadiri wanavyostahili kuishi watoto wa Mungu. Aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria: ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mtakatifu Yohane wa XXII pia aliiwaombea Watanzania paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu.
Mtakatifu Yohane wa XXIII ambaye hapo mwanzo alijulikana kama Angelo Giuseppe Roncalli, alizaliwa Novemba 25, 1881 na kufariki dunia Juni 3,1963.
Aliliongoza Kanisa Katoliki kuanzia Oktoba 28, 1958 na alitangazwa kuwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II, Septemba 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo.
Kwa mujibu wa Vatican, Waziri Mkuu Majaliwa alipata pia fursa ya kutembelea kaburi la Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye enzi za uhai wake alifanya ziara Tanzania miaka 33 iliyopita, Septemba Mosi hadi 5 mwaka 1990.
Akiwa Tanzania Papa Yohane Paulo II, alitembelea majimbo makuu Dar es Salaam, Songea, Tabora na Mwanza, pia Jimbo Katoliki la Moshi.
Mbali na kaburi la Papa Yohane Paulo II Majaliwa na ujumbe wake pia walitembelea kaburi la Baba Mtakatifu Benedikto XVI.
Baba Mtakatifu Benedikto XVI alikuwa ni Papa wa 265 kuliongoza Kanisa Katoliki, aliyetanguliwa na Yohane Paulo II na ambaye aling'atuka kabla ya kiongozi wa sasa, Papa Francis kuchukua nafasi ya kuliongoza Kanisa Katoliki duniani.
Papa Benedikto alifariki dunia Desemba 31 mwaka 2022.
https://www.vaticannews.va/sw/vatican-city/news/2023-10/waziri-mkuu-tanzania-kassim-majaliwa-atembelea-vatican.html
0 Maoni