Hot Posts

6/recent/ticker-posts

TEF wamshukuru Rais, wampongeza Mobhare

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua Mobhare Matinyi kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali. TEF pia imempongeza mteule huyo kwa kuaminiwa na Rais kushika wadhifa huo, ikieleza kuwa ina matarajio kwamba atakuwa kiunganishi kati ya vyombo vya Habari na Serikali. "TEF tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya uteuzi wa mtu sahihi kushika wadhifa huu, baada ya aliyekuwapo, ... Gerson Msigwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu,"imeeleza sehemu ya taarifa ya TEF iliyosainiwa na Mwenyekiti wake, Deodatus Balile Oktoba 2, 2023. Kupitia taarifa hiyo TEF iliongeza: "Msemaji Mkuu wa Serikali ndiye Mshauri Mkuu wa Masuala ya Habari serikalini. Tunaamini ataifanya kazi hii kwa ustadi wa hali ya juu na kwa ufasaha." Iliongeza kuwa pamoja na mambo mengine,kuna uundwaji wa vyombo vinavyoanzishwa kisheria kupitia Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kama ilivyorekebishwa mwaka 2023, jukumu ambalo lilishindikana tangu mwaka 2016. "Tunaamini sasa ni wakati mwafaka alisimamie suala hili, ili viundwe" TEF ilisema. Kuhusu uchumi wa vyombo vya habari iliosema upo katika hali mbaya na kuathiri ubora wa habari huku Serikali ikiwa ni mnufaika wa habari zinazochapishwa na kutangazwa na vyombo hivyo, TEF imesema inaamini ni wakati mwafaka wa Serikali kutenga bajeti ili kuhakikisha vyombo vya habari vinapata matangazo ya kutosha kujenga uwezo wa kiuchumi. Imesema kwa hatua hiyo na Serikali ikilipa madeni kwa vyombo vya habari ubora wa maudhui ya habari utaongezeka. "Sisi kwa upande wetu, tunamhakikishia ushirikiano wa hali ya juu. Hongera sana Ndugu Matinyi," ilihitimisha taarifa hiyo ya TEF.

Chapisha Maoni

0 Maoni