Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Serikali kupitia Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila imeisifu Menejimenti ya Hospiatali ya Rufaa ya Mkoa huo kwa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.
Nguvila ametoa sifa hizo Oktoba, 6 mwaka 2023, alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba (BRRH) na kuzungumza na watumishi wa hospitali hiyo kuhusu masuala mbalimbali ya utumishi na utendaji kazi.
![]() |
Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila akizungumza na watumishi wa Hospitali ya Rufaa Bukoba. |
“Nawapongeza watumishi wote wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba hasa Mganga Mfawidhi wa hospitali hii kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya ya kunusuru maisha ya Watanzania. Binafsi nimekuja mara nyingi katika hospitali hii kupata huduma, lakini nimekuwa nikipokelewa vizuri na majibu ya vipimo yanatoka kwa wakati, hongereni sana,”amesema Nguvila.
Ofisa Tawala huyo wa mkoa amesema kwa sasa hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba inaendelea kukua na kupanuka katika utoaji wa huduma, baada Serikali kupitia Wizara ya Afya kuleta madaktari bingwa, vifaa vya kisasa pamoja na uboreshaji wa miundombinu.
“Huduma hapa zimeboreshwa sana. Kwa sasa tumepata madaktari bingwa ambao awali hatukuwa nao, kuna vifaa vipya na vya kisasa vinavyotumika kupima magonjwa mbalimbali, mfano mashine ya CT-SCAN , vifaa vya kisasa vya upasuaji na vinginevyo, lakini pia tunaona majengo yanazidi kujenjwa na hivi punde yataanza kutumika.
"Kwa mfano, jengo la kisasa la ICU na Kitengo cha Huduma za Dharura(EMD),” amesema Nguvila.
Mbali na pongezi hizo, amewasihi watumishi wa BRRH kuendelea kufanya kazi zao kwa weledi na kuzingatia maadili ya kazi yao, sanjari na miongozo iliyowekwa na Wizara ya Afya kama ambavyo wamekuwa wakifanya kila siku, ili wananchi waendelee kufurahia huduma zinazotelewa hospitalini hapo.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Bukoba Dk. Museleata Nyakiroto, alimshukuru Katibu Tawala huyo kwa kuwatembelea na kuzungumza na watumishi kuhusu masuala mbalimbali akieleza kuwa, maelekezo yote yaliyotolewa yamepokelewa na yatafanyiwa kazi.
0 Maoni