-Yafikia asilimia 32
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), imefanikiwa kuongeza mapato (Maokoto), yake kwa asilimia 32 katika kipindi cha miaka mitatu kutoka shilingi bilioni 25.95 hadi Sh. bilioni 34.17.
Akizungumza katika Mkutano na Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam leo Oktoba 19, 2023, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, CPA Habibu Suluo amebainisha hayo.
"Katika kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa majukumu ya LATRA, mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2022/23, mapato ya yameongezeka kutoka Sh. bilioni 25.95 hadi Sh. bilioni 34.17" amesema Suluo.
Amefafanua kuwa mapato hayo ni kabla ya kukaguliwa na CAG ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 8.22 sawa na ongezeko la asilimia 32.
Katika mkutano huo ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, bosi huyo wa LATRA amesema: "Kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2021/22, mapato ya LATRA yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 25.945 hadi Sh. bilioni 28.53 ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 2.58 sawa na ongezeko la asilimia 10."
Suluo amebainisha kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2022/23, mapato ya mamlaka hiyo yaliongezeka kutoka Sh. bilioni 28.53 hadi Sh. bilioni 34.17 kabla ya kukaguliwa na CAG ikiwa ni ongezeko la Sh. bilioni 5.64 sawa na asilimia 20.
Amefafanua kuwa ingawa mapato yatokanayo na adhabu yamepungua, mapato yatokanayo na leseni yameongezeka hivyo LATRA inaendelea kufanikiwa kujenga tabia ya utii wa sheria na kupunguza adhabu kwa watoa huduma za usafiri ardhini nchini.
Akizungumzia mwaka wa fedha 2023/2024 Suluo amesema LATRA imejipanga kuhakikisha huduma bora na salama za usafiri ardhini zinawafikia wananchi, kuondoa kero na changamoto mbalimbali katika sekta.
"Hii ni katika kutekeleza maelekezo anayoyatoa Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara kwa mara," amesema. Suluo.
Kuhusu wajibu wa mamlaka hiyo kutoa, kuhuisha, kusitisha na kufuta leseni za usafirishaji, Suluo amesema LATRA hutoa leseni kila mwaka kwa vyombo vya usafiri kibiashara, baada ya mtoa huduma kukidhi masharti yanayotakiwa kwa aina ya huduma kwa kipindi cha mwaka.
"Mwaka 2020/21 hadi 2022/23, idadi ya leseni za usafirishaji ziliongezeka kutoka 230,253 hadi 284,158 sawa na ongezeko la leseni 44,205. Hilo ni ongezeko la asilimia 18.4," amebainisha Suluo.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, LATRA imeendelea kuboresha usafiri wa umma katika majiji na miji nchini ambapo imeanzisha njia mpya nane kwa Jiji la Dar es Salaam, tatu kwa Jiji la Dodoma na kufanya mabadiliko kwa baadhi ya njia za daladala jijini Arusha.
Kuhusu usafiri wa reli unaosimamiwa pia na mamlaka hiyo, Suluo ameeleza LATRA imeendelea kutoa mafunzo kwa watendaji wa TRC na Tazara, pamoja kufanya ukaguzi ili kuendelea kuhakikisha usalama wa abiria na mizigo.
"LATRA imejipanga kuendelea kufanya ufuatiliaji, maeneo yatayoangaliwa ni pamoja na madaraja, reli, mifereji ya maji, vifungashio vya reli, ushindiliaji wa kokoto kwenye tuta la reli na maungio. Hili ni jukumu la msingi kwa Mamlaka ili kuhakikisha ubora na usalama wa usafiri wa reli hapa nchini," amesema Suluo.
0 Maoni