Hot Posts

6/recent/ticker-posts

BOT yahadharisha Dola feki

-Yaeleza kukamatwa shehena kuja Afrika

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com 

Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa tahadhari kwa wamiliki wa maduka ya kubadilishia fedha na wafanyabiashara kuhusu kuwepo kwenye mzunguko kwa fedha za Marekani (Dola) zilizoisha muda wake.

Kupitia barua yake kwenda kwa benki na maduka ya kubadilishia fedha iliyo na kumbukumbu namba FD.69/130/01//61 BOT imesema, ina taarifa ya kukamatwa kwa shehena ya kiasi kikubwa cha dola zilizoisha muda wa matumizi.

Kwa mujibu wa BOT, fedha hizo zinatoka katika moja ya nchi ughaibuni, kuja Afrika.

" Kutokana na jambo hilo, benki zote na maduka ya kubadilishia fedha yanatakiwa kuchukua tahadhari zote ikiwamo kuimarisha mifumo ya utambuzi noti bandia," imetahadharisha BOT na kuongeza:

" Benki na maduka yote ya kubadilishia fedha, yanashauriwa kuendelea kuwaelimisha wateja kuhusu madhara ya kubadilisha fedha kwa kutumia mifumo isiyo rasmi ili kuepuka uwezekano wa kupewa dola feki."

Onyo hilo la BOT limekuja wakati baadhi ya wafanyabiashara wakilalamika walichodai kupungua kwa fedha hizo kwenye mzunguko, hata kuzinunua kwa masharti kwenye baadhi ya benki na maduka ya kubadilishia fedha.

Hata hivyo, taarifa ya Serikali kupitia Benki Kuu ikieleza kuwa ina akiba ya Dola bilioni 5.41 zinazotosha kuagiza bidhaa kwa miezi minne na siku 27 kuanzia Agosti 2023.

Mkurugenzi wa Utafiti na Sera wa BOT, Suleiman Misango aliwaambia wanahabari Agosti 22 kuwa upungufu wa fedha za kigeni ni himilivu.

Chapisha Maoni

0 Maoni