-Mapato yaongezeka, ufanisi wapaa
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Namba zinaipaisha Bohari
ya Dawa nchini (MSD), ndivyo unavyoweza kueleza, baada taasisi hiyo kupata
mafanikio makubwa katika utendaji wake kwa mwaka 2023.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari leo jijiniDar es Salaam, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amebainisha hayo akitaja majukumu na muundo wa bohari hiyo, pia kubainisha ongezeko la mapato yake kwa usambazaji kufikia shilingi bilioni 372.4 mwaka huu kutoka shilingi bilioni 320.9 mwaka 2022.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD), Mavere Tukai, akitoa taarifa ya utendaji, mafanikio na uelekeo wa MSD mbele ya Wahariri wa Vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam, Septemba 27,2023. |
“MSD ina majukumu manne nayo ni uzalishaji, ununuzi,
utunzaji na usambazaji, dhamira kubwa ikiwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa
za afya katika vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema Tukai wakati akitoa
taarifa ya utendaji, mafanikio na uelekeo wa MSD na kuongeza:
“MSD ina watumishi 688,magari 185 ya usambazaji,
vituo vinavyohudumiwa zaidi ya 7,600,
viwanda vya kuzalisha bidhaa za afya viwili, mizunguko ya usambazaji 6 na kanda
10.”
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, katika mwezi Agosti
mwaka huu MSD ililenga kukusanya mapato ya shilingi bilioni 35.68, hata hivyo makusanyo
halisi ni shilingi bilioni 34.08.
Akitaja mafanikio mengine mbele ya Wahariri, Tukai amesema MSD
imefanikiwa kuanzisha kitengo malum cha usimamizi na ufuatiliaji wa mikataba, kuongezeka
wa ununuzi wa bidhaa za afya kutoka kwa wazalishaji wa ndani kutoka shilingi
bilioni 14.1 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni 39.77.
“Tumeongeza zaidi mikataba ya muda mrefu kutoka
mikataba 100 yenye bidhaa za afya kwa mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia
mikataba 233 yenye bidhaa 2,209 kwa mwaka 2022/23,” amefafanua Tukai.
Katika hatua nyingine, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeipongeza MSD kwa kuvitumia viwanda vya ndani kufanikisha kazi zake, badala ya kuegemea viwanda vya nje, huku ikimpongeza Msajili wa Hazina kwa kuweka utaratibu wa taasisi zilizo chini yake kukutana na vyombo vya habari.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile wakati wa mkutano huo akieleza kuwa kufanya kazi na viwanda vya ndani vinavyozalisha bidhaa za afya ni jambo zuri linalofaa kupigiwa mfano.
"Kutumia viwanda vya ndani inasaidia kupunguza gharama hivyo kuinua uchumi wa taifa. MSD imeonesha mwelekeo mzuri katika kujali afya za watanzania kwa kuhakikisha dawa hata vitendea kazi vinapatikana," amesema Balile.
Kuhusu Msajili wa Hazina, Balile amesema: " Nampongeza ndugu yetu Nehemia Mchechu na timu yake, kwa kuanzisha utaratibu wa taasisi zilizo chini yake kukutana na wahariri na kueleza kazi zao. Hii itasaidia wananchi kuzifahamu vizuri taasisi hizo na majukumu yake."
0 Maoni