NINAWASALIMU katika jina la Mwenyezi Mungu wasomaji wote na wafuatiliaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii popote mlipo ulimwenguni na kuwakaribisha katika mtandao huu mpya kabisa wa habari DAIMATANZANIA blogspot, Online Tv na Youtube chaneli.
Ninayewakaribisha, jina langu ni Exuperius Kachenje, mwanzilishi na mmiliki wa mtanado huu, ambaye ni mwanahabari kwa zaidi ya miaka 25.
![]() |
E. KACHENJE |
Nimehudumu katika nafasi mbalimbali kwenye vyombo vya habari tofauti, kuanzia ngazi za chini hadi baraka ya kuongoza wengine kwa kuwa MPIGA PICHA MKUU, MHARIRI WA HABARI na MSANIFU MKUU WA KURASA.
Baadhi ya maeneo niliyohudumi ni upigaji picha za habari, uandishi wa habari za michezo, habari za siasa, uchumi, jamii, afya, mazingira, utawala bora, habari za uchunguzi pamoja na makala mbalimbali.
Vyombo vya habari nilivyowahi kuhudumia na nafasi nilizoshika ni pamoja na Magazeti ya Mfanyakazi (Mwandishi na Mpigapicha), Tafakari (Mwandishi na Mpigapicha Mkuu), Madaraka (Mwandishi na Mpigapicha Mkuu), gazeti la michezo Mwanasimba (Mwandishi na Mpigapicha Mkuu).
Pia nimehudumu magazeti ya Mwanaspoti na Mwananchi katika nafasi ya ripota, baadae Msanifu Kurasa, Mhariri Msaidizi, Kaimu Msanifu Mkuu magazeti ya Mwananchi Wikiendi, pia Mhariri wa Habari Gazeti la Jambo Leo.
Nimewahi kuhudumu pia Redio Tumaini katika nafasi usimamizi wa Gazeti Tumaini Letu nililoshiriki kulianzisha, pia nimekuwa mtangazaji katika Redio na Tv Tumaini na baadae Mhariri wa Habari Kituo cha Televisheni Dira na Gazeti la Dira, baadae nilikuwa Mhariri wa Habari wa Gazeti Tanzania Daima .
Ni matumaini yangu kuwa mna kiu ya kupata habari za ukweli na uhakika zilizofanyiwa kazi na waandishi na wahariri mahiri, kwa umahiri ili kukidhi na kukata kiu ya habari kwako msomaji na mfuatiliaji wa habari. Bila shaka DAIMATANZANIA ndiyo jibu la kiu hiyo.
Ni ukweli usiopingika kwamba kuna mitandao mingi ya kijamii na chaneli za mtandaoni, ambazo bila shaka zinapasha jamii habari mbalimbali. Hata hivyo, mtandao wa DAIMATANZANIA unajipambanua tofauti na vyombo vingi vya habari katika kukidhi matakwa ya wasomaji, wasilikizaji na watazamaji wa habari.
Hilo halina ubishi kutokana na ukweli kwamba katika jukumu la kuhakikisha DAIMATANZANIA tunakidhi kiu ya wasomaji wetu, sipo peke yangu, bali nipo pamoja na wanahabari na wahariri mahiri na mashuhuri.
Naamini kwa umoja, umahiri na umakini katika utendaji na timu nzima ya wanahabari kutoka mikoa mbalimbali hapa nchini, msomaji, msikilizaji na mtazamaji utapata habari kem kem, zinazokuhusu wewe au jamii inayokuzunguka.
Utapata habari za kuhusu nyumba na makazi, wafanyakazi, afya, uhifadhi maliasili,mazingira na utalii, haki za binadamu, utawala bora, demokrasia na siasa, habari za kimataifa, historia, michezo na burudani.
Tunaahidi kukupatia habari zote pamoja na zile za uchunguzi kwa kuzingatia weledi, bila upendeleo wala kuminya uhuru wa kujieleza, lakini kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.
Pamoja na hayo, tunakukaribisha wewe msomaji, msikilizaji na mtazamaji kutoa maoni yako hata kukosoa, lengo likiwa kuboresha utendaji wetu, ili kuhakikisha unaendelea kufaidi habari za uhakika na kwa wakati sahihi.
Nakusihi endelea kufuatilia mtandao huu kila wakati na kila siku, ukiwahamasisha na wengine kutufuatilia ili kwa pamoja msipitwe na habari za kina na uhakika kwa ajili ya Watanzania wote. Karibuni sana.
0 Maoni