Vijana 'Kanda Maalum' Mara kufundishwa ukarimu kwa wageni

 Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, imeanza kutoa mafunzo maalum kwa vijana wa eneo hilo ya namna ya kuwakarimu na kuhudumia wateja ili waingie katika soko la ajira hasa kuhudumia watalii katika maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri  ya Wilaya Serengeti, Victor Rutonesha akizungumza na wanahabari ofisini kwake.

 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Victor Rutonesha amebainisha hayo alipokuwa akizungumza na wanahabari waliotembelea ofisini kwake kujua namna wanavyoshirikiana na TANAPA katika masuala ya uhifadhi na utalii kwenye eneo laHifahi ya Taifa Serengeti.   

Rutonesha amesma mbinu hiyo itasaidia vijana wa Serengeti na Mkoa wote wa Mara kupata ajira kwenye kampuni mbalimbali zinazojihusisha na utalii zikiwamo hoteli na kwenye biashara zao binafsi za nje ya hifadhi.

“Tumeamua kuanzisha programu hiyo baada ya kugundua vijana wetu hapa wamepungukiwa ukarimu, hii ni kwa nia njema tu . Lakini hili pengine linatokana na mila na desturi za wenyeji wa mkoa huu, zina upungufu wa ukarimu hasa wanapohudumia wateja hata katika biashaa zao binafsi,” amesema Rutonesha.

Kwa mujibu wa Rutonesha, wamegundua kuwa wasipofanya hivyo uwekezaji utakapoanza na kushamiri, utawaacha nje vijana wa mkoa huo kutokana na sababu mbalimbali, kikubwa kikiwa ni mila, desturi na mazoea ya wenyeji wa mkoa huo.

“Kwa mfano baadhi ya mila za baadhi ya makabila ya mkoa huu zinakataza mwanamke kumtuma mwanaume kwa kudhani kwamba amemdharau. Mwanamke anaweza kwenda dukani au hotelini akamtuma mhudumu wa kiume amletee soda ainafulani,lakini yule mhudumu akalete soda aina nyingine akaifungua na kumpa mteja huku akimwambia kunywa hiyo ndio iliyopo, uliyotaka hakuna. Hayo yametokea, jambo ambalo linawafanya vijana kushindwa kuajirika katika kampuni hasa zinaongozwa na wanawake,” amesema.

Rutonesha ameongeza: “Vijana wengi wanaishi kwa mazoea ya tamaduni zao, hawajui umuhimu wa kujali mteja katika biashara zao. Matokeo ya hali hiyo, vijana wanaofanyakazi kwenye hoteli na kampuni za utalii wilayani Serengeti wanatoka Kilimanjaro na mikoa mingine.Kwa sababu hiyo, sisi viongozi hatuwezi kuacha haya yaendelee.”

Amesema wameanza kuwapa elimu vijana na akina mama wanaozungukwa na Hifadhi ya Taifa erengeti na maeneo mengine kwa sababu uwekezaji wa mahoteli makubwa na biashara mbalimbali zinaanza kufunguliwa.

Akizungumzia miradi inayotarajiwa kuchochea fursa za kiuchumi wilayani humo, Kaimu Mkurugenzi Rutonesha amesema kwa sasa hoteli nyingi za kitalii zitajengwa kwenye vijiji vinavyopakana na hifadhi ambavyo tayari vina mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Ingawa hakutaja idadi ya hoteli zinazotarajiwa kujengwa maeneo hayo ya vijiji, amesema halmashauri inaendelea kupokea maombi ya watu wanaotaka kuwekeza hoteli zikiwamo zenye hadhi ya nyota tano na biashaa nyingine kubwa.

Kaimu Mkurugenzi huyo wahalmashauri amesema biashara hizo kubwa zitakuwa kwenye maeneo ya wananchi ambao vijiji vyao vimetenga maeneo ya uwekezaji na utalii kwa ujumla, hivyo wakazi na wenyeji wa maeneo hayo hawana budi kujiandaa kupokea na kufanya biashara na wageni kwa lugha ya ukarimu na uaminifu.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi