PPP Center yapika wataalam miradi ya ubia
- Lengo kupata miradi yenye tija,kuipunguzia mzigo Serikali
Mwandishi Wetu, Arusha
Kituo cha Ubia kati Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, kinaendesha mafunzo maalum ya ubobezi wa PPP kwa hatua tatu tofauti.
Hatua hizo ni Ngazi ya Msingi, Utayarishaji Miradi na Uendeshaji pamoja na Usimamizi Miradi ya PPP, ili kuwajengea uwezo watumishi katika kuibua na kuchakata miradi ya maendeleo yenye tija kwa utaratibu PPP.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Miradi wa PPP-Center, Dk. Suleiman Kiula |
Uendeshaji wa mafunzo hayo ambao ni jukumu la Kisheria
la Kituo hicho cha Ubia, yana lengo la kuongeza wataalam zaidi, watakaoweza
kutayarisha miradi ya PPP yenye tija kwa ufanisi itakayokuwa kivutio kwa wawekezaji
kutoka sekta binafsi ndani na nje ya nchi, hivyo kuipunguzia Serikali mzigo wa
bajeti ya maendeleo.
Mafunzo hayo kwa Hatua ya Uandaaji Miradi yamefanyika
mkoani Arusha kwa siku 10 mapema mwezi huu wa Juni, yakiwajumuisha watendaji
kutoka sekta mbalimbali za umma Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo washiriki wanaofaulu
mitihani iliyotolewa Taasisi Maalum inayoratibu Mitalaa ya PPP Duniani (APMG),
watatunukiwa vyeti vya ubobezi wa miradi ya PPP kwa hatua husika.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo,
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Miradi wa PPP-Center, Dk. Suleiman
Kiula, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya wajibu wa kisheria wa PPP Center katika
kuwajengea uwezo wa utendaji watumishi wa umma na binafsi katika eneo hilo la
PPP.
“PPP Center, kinatekeleza wajibu wake kisheria. Kwa mwaka huu 2025 mafunzo haya ni hatua ya pili. Hatua za kwanza zilifanyika Agosti 2024 na Aprili mwaka huu,ambapo takriban washiriki 90 kati ya 180 wamefaulu mitihani ya APMG,” alisema Dk. Kiula.
Alisema lengo la kuandaa wabobezi wa miradi ya
PPP ni kutanua wigo wa Bajeti ya Serikali katika miradi inayogusa jamii moja
kwa moja ikiwamo ya huduma za jamii na miundombinu, kuongeza ufanisi na kuvuna
teknolojia mpya ya kisasa.
Alifafanua kuwa hatua hiyo ya pili kati ya tatu
za mafunzo hayo, ilijumuisha washiriki 80, ambao nao mwishoni mwa mafunzo wametapimwa
kwa mitihani ya ubobezi ya APMG na waliofaulu kutunukiwa vyeti vya ubobezi wa
PPP hatua ya pili.
Kwa mujibu wa Dk.Kiula mafunzo hayo
yataliwezesha taifa kupata miradi yenye ubora katika kufikia malengo la Dira ya
Taifa ya Maendeleo ya 2025-2050 iliyotokana na maoni ya wananchi, ikichagiza
Tanzania kufikia lengo la Uchumi wa Dola trilioni moja na pato Dola kati ya
4500 hadi 7,000 kwa kila Mtanzania.
“ Ili kufikia huko, ndio sababu kunahitajika
sekta binafsi kujumuishwa katika miradi ya miundombinu na huduma kwa jamii
ambayo itaratibiwa kwa Ubia kati ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), inayosimamiwa
na PPP Center chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake, David Kafulila,” alisema
Mkufunzi wa Mafunzo hayo Jan Willem Middelburg ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Cybiant ya Uholanzi, alisema PPP Center imechukua hatua muhimu ya kutoa mafunzo hayo kwa watendaji wa umma na sekta binafsi kwa kuwa kasi ya maendeleo ya dunia ya sasa inaendana na uhitaji wa wataalam sahihi wa kusimamia miradi ya ubia ili kuleta maendeleo ya taifa kwa haraka.
Washiriki wa mafunzo ya ubobezi wa miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi wakiwa katika picha ya pamoja. |
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Asia
Mohammed Haji kutoka Kamisheni ya Miradi ya Ubia Kati ya Umma na Sekta Binafsi
(PPP)Zanzibar, alisema: “Mafunzo haya yametupa mwanga na kutambua namna bora ya
kuchakata miradi ya ubia na Serikali inavyoweza kuepuka vichocheo vya
kukwamisha miradi ya maendeleo.”
Mshiriki mwingine, Evelyne Magambo alisema mafunzo hayo ni chachu ya mabadiliko katika kusimamia miradi ya Serikali ili jamii inufaike nakuliongezea taifa kasi ya maendeleo.
Mkufunzi wa Mafunzo hayo Jan Willem Middelburg ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Cybiant ya Uholanzi(Kulia) akiteta jambo na mmoja wa waratibu wa mafunzo hayo Angel Musahara kutoka Benki ya Dunia |
Maoni
Chapisha Maoni