Wanyama 400 wauawa Mikumi

 -Kamera kunasa wahalifu

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Hifadhi ya Taifa Mikumi inajipanga ili kuweka  kamera zikazowekwa geti la kuingilia hifadhi hiyo eneo la Kijiji cha Doma, Mikumi Mjini inapoishia hifadhi kwenye barabara Kuu kwenda Iringa, inayopita hifadhini humo, ikielezwa kuwa wastani wa wanyama 400 hufa kwa kugonjwa na gari kila mwaka.

Kamishna Augustine Masesa

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Kamishna Augustine Masesa amesema hayo Juni 28/2025 akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwanasa madereva watakaowagonga wanyama kwenye eneo la hifadhi na magari yanayovunja sheria kwa kutembea mwendo usioruhusiwa.

 Alikuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu hifadhi hiyo, ambapo amesema mradi huo unahitaji takriban shilingi bilioni 2.

“Tayari upembuzi yakinifu umefanywa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP), tunasubiri pesa tu ipatikane kutekeleza mradi huo kwenye eneo hilo la kilometa 50 inapokatiza baabara kuu hifadhini,”ameseme Kamishna Masese.

Kamishna Masesa amesema hatua hiyo ina lengo la kuondoa tatizo la wanyama kugongwa na magari na wahusika wengi kukimbia.

“Katika barabara kuu inayopita ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi kuelekea Iringa, kila siku anagogwa mnyama, kila mwaka mmoja wastani wa wanyama 500 hugongwa na magari na kupoteza maisha, kisa madereva wasiozingatia sheria, lakini pia watu wanaotupa taka hifadhini,” amesema Kamishna Masesa .

Amesema kwamba katika kukabiliana na tatizo hilo kwa sasa wameanza kufanya doria ili kubaini wanaogonga wanyama na wanaotupa taka kwani husababisha nyani wengi kugongwa kutokana na kufuata taka hizo barabarani.

“Anayegonga mnyama tukimkamata lazima alipe faini, hii inategemea amemgonga mnyama aina gani.Wapo tuliowakamata na magari yao, wameshindwa kulipa faini na kutelekeza magari hayo,” amebainisha mkuu huyo wa Hifadhi ya Taifa Mikumi.

Akitoa mfano amesema kwa wanaogonga Twiga, faini inafikia Dola za Marekani 20,000 ambazo ni zaidi ya Shilingi milioni 50.

“Hapa dereva jiulize, kwa nini uingie kwenye matatizo kama hayo badala ya kufuata sheria zilizopo? Nawahiiza madereva kufuata sheria wanapopita eneo la Hifadhi ya Taifa Mikumi,” amesema.

Muikolojia wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, Peter Mathew Jacob (Pichani chini), amesema kwa wastani kila mwaka takriban wanyama 400 hugongwa na magari yanayopita hifadhini, ingawa idadi ya wanyama wanaogongwa kwa mwezi hutofautiana nyakati za masika na kiangazi.

"Ukubwa wa tatizo unatofautiana kulingana na msimu, msimu wa kiangazi tunakuwa na maeneo machache yenye maji hivyo wanyama wengi huvuka kutafuta maji na kugonjwa na magari," amesema Jacob na kufafanua:

"Kiangazi tunakuwa na wastani wa wanyama 17 hadi 20 wanaogongwa, masika  wanagongwa saba hadi 15, hata hivyo takwimu za karibuni kwa mwaka 2021/2022 zinaonyesha  waligongwa wanyama wengi zaidi,waligongwa 482."
 
Katika hatua nyingine Kamishna Masesa ameishukuru Serikali kwa kuziachia hifadhi za taifa asilimia 51 ya makusanyo yake ili kuendesha shughuli za maendeleo hifadhini. 

“Tunaishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, sasa tutaacha kutegemea fungu kutoka serikalini, naamini hatua hii inatokana na moyo na utendaji wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA),” amesema Kamishna Masesa

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi