Hot Posts

6/recent/ticker-posts

'Wataalam Posta tumieni maendeleo teknolojia kufungua fursa za kiuchumi'

 MWANDISHI WETU, WHMTH, Arusha

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa, amewataka wataalamu wa masuala ya Posta Afrika, kutumia vyema maendeleo ya teknolojia katika kuwezesha sekta hiyo kufungua fursa za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo.

Washiriki wa vikao vya Kamati za Wataalamu wa Masuala ya Posta kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU0, uliofanyika jijini  Arusha, Juni 3, 2024. vikao hivyo ni vya utangulizi kabla ya Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU litakalofanyika Juni 11 hadi 12 jijini humo. 

Dk. Mndewa amesema hayo Juni 03, 2024 mkoani Arusha wakati akifungua Vikao vya Kamati za wataalamu wa masuala ya posta kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), ikiwa ni vikao vya utangulizi kabla ya Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU litakalofanyika Juni 11 hadi 12 jijini humo.

Amesema kuwa ili nchi za Afrika ziweze kufanikiwa zaidi katika masuala ya Posta na kuendana na kasi ya ukuaji wa Biashara Mtandao, nchi wanachama kwa pamoja zina wajibu wa kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchumi wa kidigitali. 

"Ni wajibu wetu kuhakikisha tunatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili nchi wanachama, kwani  bado kuna changamoto kwenye nchi za Afrika, ikiwemo miundombinu na teknolojia, zinazohitaji  kupatiwa ufumbuzi ili kurahisisha mawasiliano kwa haraka," amesema Dk.Mndewa. 

Amebainisha kuwa ni vema nchi za Afrika kwa umoja wao zikahakikisha zinatumia teknolojia ili kupunguza gharama na kutimiza malengo ya nchi waliyojiwekea ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia yanayoshuhudiwa kote duniani.

Naye Katibu Mkuu wa PAPU, Dk. Sifundo Chifu Moyo amesema, zipo changamoto kadhaa zinazokabili sekta ya Posta zinazowafanya wateja kutokuwa na furaha, lakini kwa sasa kwa asilimia kubwa viongozi wa nchi hizo wameanza kuzitafutia ufumbuzi.

Ametaja moja ya changamoto kuwa ni kutikisika kwa Mauzo ya Hisa katika Soko na kushuka kwa mapato hivyo, vikao vya kamati hizo  za wataalamu, vinatarajiwa kutoa majawabu ya namna teknolojia inavyoweza kuwa suluhu ya changamoto hizo ili kurejesha imani ya wananchi katika sekta hiyo.

“Kama wote mnavyoelewa, teknolojia haimilikiwi na mtu yeyote. Kwa hiyo kila mmoja ana fursa ya kuitumia vizuri teknolojia ili kujikwamua kiuchumi na sekta ya Posta haipaswi kuwa nyuma. Kwa sasa Posta inaichukulia teknolojia kwa uzito mkubwa na ipo kwenye sera zake, pia inahakikisha teknolojia inapelekwa karibu zaidi na wananchi,” amesema Dk. Moyo.

Amesema ana furaha kwa kuwa baada ya miaka arobaini kwa mara ya kwanza mkutano huo unafanyika katika jengo la PAPU, ambalo ni moja ya vitega uchumi na kielelezo cha uwepo wa PAPU ambalo litadumu kwa miaka mingi ijayo kuonyesha uhai wa sekta ya Posta.

Chapisha Maoni

0 Maoni