Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha
Wakati vikao vya Kamati za Ufundi vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), vikiendelea kwa siku ya tatu jijini Arusha, Tanzania imetoa msimamo wake baada ya kuwasilisha hoja zake ikiwemo inayopendekeza kuwa na mwakilishi kiongozi katika nafasi ya juu ya uongozi wa umoja huo.
![]() |
Baadhi ya wawakilishi wa Tanzania kwenye mkutano wa Kamati za Ufundi vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), vinavyoendelea kwa siku ya tatu jijini Arusha. |
Wawakilishi wa Tanzania wametoa msimamo huo wakizingatia kwamba kwa mujibu wa mkataba wa PAPU, nchi mwenyeji ambayo kwa sasa ni Tanzania inalazimika kuchangia asilimia 50 ya bajeti ya uendeshaji ya umoja huo kila mwanzo wa mwaka wa fedha, iwapo nchi wanachama hazijachangia kwa wakati, fedha ambazo baadaye hurejeshwa.
"Katika hoja zetu, tumesisitiza Tanzania kupatiwa nafasi hiyo ili kuhakikisha usimamizi imara wa fedha zinazotolewa, ambazo Tanzania imekuwa ikilipa kama nchi mwenyeji, pia kusimamia kikamilifu, ili kupata marejesho ya gharama za ujenzi tulizolipa zaidi ya kiwango cha umiliki cha asilimia 40 kilichowekwa," alisema mmoja wa wawakilishi wa Tanzania katika mkutano hu, akioomba jina lihifadhiwe kwa kuwa sio msemaji.
Wawakilishi hao wa Tanzania wametoa pendekezo hilo la kuwa na mwakilishi kwenye nafasi ya juu ya uongozi wa PAPU, Juni 5, 2024 mbele ya Kamati ya Fedha na Utawala katika vikao vya Wataalam wa Masuala ya Posta vinavyoshirikisha wajumbe kutoka mataifa 46 wanachama wa PAPU.
![]() |
Wawakilishi wa mataifa mbalimbali wakifuatilia mkutano wa Kamati za Ufundi vya Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika (PAPU), vinavyoendelea kwa siku ya tatu jijini Arusha, Juni 5,2024. |
Katika hatua nyingine, kwenye Kamati ya Mkakati , wajumbe wa Tanzania walibainisha mchango mkubwa wa Tanzania katika ujenzi wa jengo la PAPU lililopo jijini Arusha, ambapo mwaka huu 2024 unafanyika Mkutano wa 42 wa Baraza la Umoja wa Posta Afrika.
Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo imeazimia kuunda Kikosi Kazi katika Kamati ya Mkakati, kitakachoshughulikia upanuzi na ushirikishaji watoa huduma katika Sekta ya Posta, ambapo Tanzania imejitolea kushiriki pamoja na nchi za Botswana, Burkina Faso, Cameroon, DRC, Ivory Coast, Kenya, Misri, Namibia, Niger na Uganda.
Wajumbe hao pia wamejadili masuala ya mapato na matumizi ya umoja, miradi, ajira na stahiki za watumishi wazawa, michango ya ada za uanachama na Mpango Mkakati wa miaka minne wa sekta ya posta barani Afrika, ili iweze kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.
0 Maoni