Hot Posts

6/recent/ticker-posts

LHRC yachambua sheria uchaguzi

-Yataka Muswada Katiba bungeni

 
 Mwandishi Wetu, daimatzanews@gmail.com 

KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimechambua Sheria za Uchaguzi zilizosainiwa hivi karibuni na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kikieleza kuwa kimehusika kikamilifu katika jitihada za uchechemuzi na maboresho ya mfumo wa uchaguzi na vyama vya siasa nchini, huku ikitoa wito kwa Serikali kuwasilisha Bungeni Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kwa manufaa ya watanzania.

 Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Aprili 4, 2024 mbele ya wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga amebainisha kwamba kituo hicho kilihusika katika mchakato wa maboresho ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya 2024, Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya 2024, Sheria ya Vyama vya Siasa na Gharama za Uchaguzi, zilizopitishwa na Bunge kisha kusainiwa na Rais.
Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk. Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 4, 2024 jijini Dar es Salaam.

 "Tamko hili linatolewa kwa msingi kwamba, LHRC ni mdau katika haya, ilifanya uchambuzi na baadaye kuwasilisha maoni mbale ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria jijini Dodoma, lakini kuna mambo saba ya msingi yaliyopendekezwa na wadau yameachwa kando, " amesema Dk. Henga ambaye pia ni wakili. 

 Dk. Henga amesema kuwasilishwa kwa miswada hiyo kulileta matumaini mapya kwa Taifa kutokana na kuwepo hitaji la maboresho ya mfumo wa uchaguzi na vyama vya siasa la muda mrefu. 

 Kuhusu Katiba, Dk Henga amesema LHRC inaendelea kutoa wito kwa Serikali kuwasilisha Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ili kufanikisha lengo la maboresho yanayotarajiwa, kama ilivyopendekezwa na wadau, pamoja na mapendekezo ya Ripoti ya Kikosi Kazi cha Demokrasia ya Vyama Vingi, iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kikosi hicho, Profesa Rwekaza Mukandala, Oktoba 21, 2022.

 Akizungumzia zaidi sheria hizo zilizokwishafanyiwa marekebisho, Dk. Henga amesema LHRC imebaini kuwepo kwa mambo hayo ambayo walipendekeza yaondolewe kwenye sheria hizo, lakini bado yapo ikiwamo watumishi wa umma kuendelea kuwa sehemu ya Tume ya Uchaguzi pamoja na maamuzi ya tume na matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani.

Dk. Henga amesema miongoni mwa mambo ambayo LHRC na wadau wengi walishauri ni Tume ya Uchaguzi kuajiri watumishi wake yenyewe, ili kuipa uhuru wa kutosha katika utekeleza wa majukumu yake na kuongeza uaminifu kwa wadau wa uchaguzi. 

Kwa mujibu wa LHRC pendekezo hilo halikuchukuliwa, badala yake watumishi wa umma wameendelea kuwa sehemu ya Tume ya Uchaguzi. 

“Mathalani, kifungu cha 6 cha Sheria, imeondoa neno Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji na kuweka neno watumishi wa umma waandamizi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.
Pia kifungu cha 7 cha sheria kimeendelea kuwatambua Wakurugenzi wa Halmashauri kuwa maofisa uandikishaji wapiga kura,  kifungu cha 8 kimeendelea kuwatambua watumishi wa umma kuwa waratibu wa uchaguzi katika ngazi za mikoa,” amesema.

Akifafanua, amesem kwa tafsiri ya kisheria, Wakurugenzi wa Halmashauri kwa nafasi zao ni watumishi waandamizi wa umma, hivyo licha ya kutotajwa kwa nafasi zao, bado wanaweza kuwa wasimamizi wa uchaguzi, jambo ambalo linaendelea kutotibu, wala kuleta afueni ya mifumo ya uchaguzi, ambayo imekuwa ikilalamikiwa kwa muda mrefu.

Amesema katika eneo ambalo LHRC na wadau wengine wa demokrasia walipendekeza ni matumizi ya teknolojia katika mchakato wa uchaguzi kwenye hatua zote, yaani uandikishaji, uchukuaji na uwasilishaji wa fomu za uteuzi wa wagombea, upigaji kura na kutangazwa kwa matokeo. 

“Kwa mfano, vifungu vya 12, 16(5), 34(2) a 50(7) vya sheria tulipendekeza uandishikishaji na uwasilishwaji wa fomu za wagombea ufanyike kwa njia za kielektroniki. Hata hivyo baada ya kupitishwa kwa sheria hii tumebaini kuwa kifungu kimepitishwa kama kilivyokuwa awali  kwenve muswada," amesema na kuongeza:

“Eneo lingine ni kifungu cha 166 kinachoweka matumizi ya teknolojia kuwa hiari, hapo LHRC na wadau wengine tulipendekeza matumizi ya teknolojia kwa mujibu wa kifungu cha 166 cha sheria kuwa ya lazima, lakini baada ya kupitia sheria iliyopitishwa tumebaini kuwa kifungu hiki kimebaki kama kilivyo.”

Kuhusu suala la mgombea binafsi, Dk. Henga amesema licha ya kuwepo kwa maamuzi mbalimbali ya Mahakama za ndani na za kikanda zilitoa uamuzi wa kuwepo wa mgombea binafsi, bado kumekuwepo na kusita kufanya uamuzi wa kurekebisha Katiba na sheria juu ya suala hilo.

“Kwa mfano Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu katika shauri Mchungaji Christopher Mtikila dhidi ya Serikali ya Tanzania!, kwa mujibu wa Ibara ya 39(1) (c) na Ibara ya 671) ( b) pamoia na masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 1979, mtu hatakuwa mwanachama wa chama cha siasa, Sifa za kuchaguliwa kuwa Rais, Mbunge au diwani isipokuwa kama ni mwannachama wa chama cha siasa.

“Mbunge au diwani ni lazima awe anatokana na chama cha siasa, hii inathibitisha kutochukuliwa kwa maoni ya wadau tuliotaka uwepo wa mgombea binafsi, licha ya LHRC na wadau wengine kupendekeza mabadiliko madogo ya Katiba Katika ibara za 67(0)(b) na 39(1)(c) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ili kuruhusu uwepo wa mgombea binafsi, lakini bado Serikali haijafanyia kazi,” amesema

Amesema ni imani yao kwamba, uwepo wa mgombea binafsi utatachochea ukuaji wa demokrasia nchini pamoja na kuongeza wigo wa watanzania kuwa na haki ya kuchaguliwa bila kulazimika kupitia mkondo wa vyama vya siasa.

Hata hivyo, amesema kwa upande mwingine, LHRC na wadau walipendekeza maamuzi ya Tume ya Uchaguzi kuhojiwa Mahakamani kwa njia za mapitio au mashauri ya kikatiba, hata hivyo bado maamuzi ya tume yatakuwa ya mwisho na hayatahojiwa Mahakamani. 

“Pia moja ya eneo ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa muda mrefu ni vyombo vya habari kutotenda haki kwa wagombea wote kwa usawa wakati wa urushaji wa matangazo na vipindi vya kampeni. 

“Kumekuwa na malalamiko kwa vyombo va habari kupendelea wagombea wa upande mmoja hii ilitokana na upungufu uliopo katika sheria zetu za uchaguzi kutokuwa na mifumo ya kuviwajibisha vyombo vya habari vinavyokiuka taratibu wakati wa kampeni,” amesema.

Kuhusu matokeo ya urais kutohojiwa mahakamani, amesema kwa mujibu wa ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iwapo mgombea wa kiti cha urais atatangazwa na Tume ya uchaguzi kuwa ameshinda ushindi wake hautahojiwa mahakamani.
Dk.Anna Henga

“Tunatambua kuwa sharti hili ni la kikatiba hivyo ili kufanyiwa marekebisho ni lazima tufanye mabadiliko madogo ya katiba ili kuifanya marekebisho ibara ya 41(7) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 ili matokeo ya Urais yaweze kuhojiwa mahakamani,” amesema

Hata hivyo amesema LHRC imebaini masuala chanya kadhaa yaliyomo katika Sheria hizo mpya ambayo ni pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri za Manispaa, Jiji na Wilaya kuondolewa kuwa wasimamizi wa uchaguzi ingawa wamebaki kuwa waandikishaji wa uchaguzi.

Amesema sheria pia imeweka sifa ya mtu kuwa msimamizi wa uchaguzi; (i) awe hajawahi kutiwa hatiani katika shauri la nidhamu au kosa lolote la jinai; awe hajawahi kuadhibiwa kwa kifungo kinachozidi miezi sita (6) na hajawahi kuwa kiongozi wa chama cha siasa.

“Pia sheria imefuta suala la wagombea kupita bila kupingwa katika ngazi zote (Rais, Ubunge na Madiwani), sharti la Mwenyekiti, Makamu Mwenyetiki na waiumbe wa Tume ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji Kusimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi kufutwa kwa sharti la kulipia ada yakupata upya kadi ya mpiga kura iliyoharibika au kupotea,” ameongeza.

Aidha ametoa wito kwa serikali kuwasilisha muswada wa sheria utakaotoa fursa ya kufanya mabadiliko ya katiba ili kuruhusu baadhi ya masuala ambayo kwa uasili wake hayawezi kufanyiwa marekebisho bila kugusa Katiba.

Mwisho

Chapisha Maoni

0 Maoni