-13% pekee wana uhakika wa kipato
-Wewe upo kundi gani?
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Asilimia 15 ya Watanzania, wanaishi kwa kutegemea pesa za kupewa kwa kutumiwa au kudakishwa kama magolikipa kutoka kwa ndugu, jamaa, au marafiki, ili kuendesha maisha yao ya kila siku, utafiti umebainisha.
Taarifa ya utafiti unaojulikana kwa jina la Finscope Tanzania 2023, ambao umetolewa na Wizara ya Fedha hivi karibuni imebainisha hayo na kwamba fedha hizo hutumwa kupitia mifumo rasmi iliyopo.
FinScope Tanzania ni utafiti wa kina wa mahitaji ya sekta ya fedha kwa watu wazima Tanzania, walio na umri wa kuanzia miaka 16 na kuendelea.
Umeonyesha pia kwamba, asilimia 13 pekee ya Watanzania, ndio wenye vyanzo vya mapato vinavyowalipa kwa uhakika, mara kwa mara.
Utafiti huo uliolenga kujua na kutoa taarifa za hali ya matumizi ya huduma za fedha nchini, unatajwa kuwa ni kipimo cha kuaminika kubaini mahitaji na matumizi ya huduma za fedha kwenye makundi mbalimbali ya watu.
Matokeo ya utafiti huo, yamekuja huku idadi ya Watanzania kwa mujibu wa Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 ni takriban milioni 61, kati ya hao vijana wanatajwa kufikia takriban asilimia 40.
Pamoja na mambo mengine ripoti hiyo ilitafuta kujua mtu binafsi anazalisha mapato na kiasi gani cha fedha hupokelewa kupitia vyanzo hivyo na matumizi kupitia mifumo hiyo.
Majibu ya utafiti huo yalibainisha: “ Asilimia 15 hutegemea mtu au watu wengine kumpa au kumtumia pesa; Asilimia 35 hupata kipato chao kwa kufanya kazi za hali ya chini au vibarua vya msimu, huku asilimia 44 ya Watanzania wakipata fedha kutokana na biashara au kilimo, yote yakiwa ya msimu.”
Ikieleza zaidi taarifa ya Finscope imesema: “Ni asilimia 13 tu ya Watanzania ambao vyanzo vyao vya mapato huwalipa mara kwa mara.”
Utafiti huo umeeleza kwamba, changamoto zilizopo sasa zinatokana na sababu mbalimbali ikiwamo jinsi watu wanavyotafuta na kupata mapato yao ukibainisha kuwepo kwa ukiukwaji wa taratibu katika vyanzo vingi vya mapato, ambazo sekta ya fedha inatakiwa kuzifanyia kazi kuziondoa.
Utafiti huo unaacha swali kubwa kwa Watanzania kila mmoja kujiuliza, ameangukia kundi gani katika mgawanyo huo kuhusu kipato.
Finscope ni utafiti ulioshirikisha sekta ya umma na binafsi, unaoongozwa na Wizara ya Fedha Tanzania Bara na Zanzibar na Benki Kuu ya Tanzania, ili kukuza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), ukiihusisha Ofisiya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS).
FinScope Tanzania 2023 ni utafiti wa tano kaufanyika, nyingine zilifanyika mwaka 2006, 2009, 2013 na 2017.
0 Maoni