-Ni Homa ya Moyo ya Rumatiki
-Wataalam wasema unaongoza kwa vifo
-Waitana Abu Dhabi kuujadili
NI pigo, ni hatari mpya kiafya. Ndivyo unavyoweza kusema kwa kifupi, baada ya wataalam wa afya kubainisha uwepo wa Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki nchini, unaotajwa kuongoza kwa kusababisha vifo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mahojiano maalum na DaimaTanzania mapema juma hili jijini Dar es Salaam, Profesa Pilly Chillo wa Kituo cha Umahiri cha Kufundishia na Kufanya Tafiti za Magonjwa ya Moyo cha Afrika Mashariki na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk.Samwel Rweyemamu wamebainisha tatizo hilo, wakieleza ni kubwa.
Wataalam hao wamesema ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki unaogoza kwa kusababisha vifo kutokana na matatizo ya moyo kushindwa kufanya kazi vizuri kitaalam 'Heart failure'.
Mahojiano na wataalam hao yamefanyika kwa nyakati tofauti katika taasisi ya moyo JKCI na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Mloganzila.
Dk. Rweyemamu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), amesema:
" Wanaofanyiwa upasuaji ni wengi. Huwapata watoto wa kuanzia miaka mitano hadi 15, lakini hata wenye umri zaidi ya huo wanapata."
Naye Profesa Chillo amesema: "Ni ugonjwa ambao hushambulia na kuathiri valvu za moyo (heart valves), hivyo kuufanya ushindwe kufanya kazi yake ya kusukuma damu vizuri. Hii husababisha mgonjwa kupata dalili za Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki, ikiwamo kushindwa kupumua vizuri, kuchoka sana,miguu na tumbo kujaa maji na zinazofanana na hizo."
Hata hivyo, wamesema ugonjwa huo si mpya, bali ulikuwepo miaka mingi iliyopita, hata nchi zilizoendea, lakini kutokana na maendeleo huko umetoweka.
Serikali, asasi za ndani na nje
Tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) kwa kushirkiana na Shirika la Afya Duniani(WHO) ilishaanza kuchukua hatua kwa kukutanisha wadau mbalimbali wapatao 30 kujadili kuhusu ugonjwa huo, hali halisi na hatua za kuchukua Juni 21, 2021.
Katika mkutano huo, ilielezwa kwamba watoto 21 kati ya kila 1,000 huku uwiano wa uwezekano wa maambukizi ukielezwa kuwa ni wastani asilimia 2.1.
Kama ilivyo kwa Tanzania nchi za Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla wameanza kuchukua hatua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa huo unaoshika kasi.
Mapema Oktoba 9,2023, Chama cha Madaktari wa Moyo wa Afrika (PASCAR), chini ya Mwenyekiti wake Dk. Emmy Okello kutoka Uganda, kilifanya mkutano maalum na waandishi wa habari wa Afrika kwa njia ya mtandao, ili kuwaelimisha kuhusu ugonjwa huo na umuhimu wa kutumia vyombo vya habari kuelimisha jamii kuhusu Homa ya Moyo wa Rumatiki, hivyo kuiokoa.
Hilo lilifanyika baada ya wataalam hao kubaini ongezeko la kasi la wagonjwa hasa watoto wanaofanyiwa upasuaji wa kuzibua valvu za moyo zilizoziba kutokana na ugonjwa huo hatari.
Mkutano huo ulifanyika ukitanguliwa na maadhimisho ya Siku ya Moyo Duniani, Septemba 29, huku wataalam hao wakiitana kwa Mkutano Mkuu wa Kitaaluma kuhusu Magonjwa ya Moyo utakaofanyika Novemba 2 hadi 4, Abu Dhabi, yote ikitajwa ni mwendelezo wa juhudi za kuiamsha dunia ifahamu zaidi kuhusu Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki, mkutano unatotarajiwa kuonyesha njia bora zaidi kuudhibiti.
Ukubwa wa tatizo
Kuhusu ukubwa wa tatizo Profesa Chillo mtafiti mwandamizi ambaye pia ni mmoja wa watafiti wa awali wa tatizo hilo nchini amesema: " Ugonjwa huu ni tatizo kubwa nchini kwani ndio unaoongoza kwa kusababisha vifo vitokanavyo na matatizo ya moyo kutofanya kazi vizuri kwa watoto na vijana chini ya miaka 35. Pia ndio unaoongoza kusababisha upasuaji mkubwa wa moyo nchini.
Kule Mkoa wa Manyara asilimia 52 ya watoto waliopimwa wamebainika kuwa na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Dk. Rweyemamu anasema upo zaidi maeneo na mikoa ya wafugaji, akieleza asilimia tatu ya watoto wanaougua mafindofindo mara kwa mara wana hatari ya kuugua Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki.
"Kama nilivyosema upo zaidi mikoa ya maeneo ya wafugaji, Karatu kule Manyara kunaongoza kwa wagonjwa wengi, upo Mkoa wa Singida, Dodoma hata Dar es Salaam ingawa hakuna wafugaji wengi," anasema Dk. Rweyemamu.
Akizungumzia sababu za Ugonjwa wa Moyo wa Rumatiki, Profesa Chillo ameeleza husababishwa na vimelea vya bakteria aina ya Streptococcus, alivyovielezea kuwa husababisha mafindofindo, hasa kwa watoto wadogo chini ya miaka 15.
"Kwa baadhi ya watoto, mafindofindo yanaweza kusababisha kupata homa ya Rumatiki (rheumatic fever), ambayo hushambulia na kuathiri vali za moyo," ameeleza mtaalam huyo.
Naye Dk Rweyemamu anasema ugonjwa huo una sababu nyingi zikiwamo za umasikini huku waathirika wakuu wakiwa watoto na akina mama.
"Katika nchi nyingi zilizoendelea, ugonjwa huu hakuna. Nasema una sababu za kimasikini kwani huweza kusambaa maeneo ambapo watoto wanalala wengi kwenye chumba kimoja, maeneo kama hosteli au nyumba zisizo na madirisha au zisizoruhusu hewa ya kutosha kama zile nyumba za tembe za wafugaji," anasema Dk. Rweyemamu.
Je, utajuaje mtoto ana ugonjwa huo kutokana na Streptococcus?
Akijibu swali hilo, Profesa Chillo analeza kuwa dalili za mafindofindo ni koo kuuma, homa, sauti kukauka, wakati mwingine mafindofindo kuwa na usaha."
Hata hivyo, anasema ni vigumu kutofautisha dalili za mafindofindo yatokanayo na bakteria aina ya Streptococcus na yale yatokanayo na virusi.
Dalili
Akieleza kuhusu dalili za Homa ya Moyo ya Rumatiki, Profesa Chillo anasema hutokea kati ya wiki mbili hadi nne baada ya mtoto kupata mafindofindo yatokanayo na bakteria aina ya Streptococcus.
Amezitaja kuwa ni pamoja na homa kali, viungo kuuma na pia kuvimba, matatizo kwenye ngozi na moyo kwenda mbio.
Naye Dk. Rweyemamu anaongeza: "Homa ya Moyo ya Rumatik (HMR) au kitaalam RDH inapompata mtu ni dalili za moyo kushindwa kufanya kazi."
RDH na Malaria
Wataalam hao wametahadharisha kuwa mara nyingi Homa ya Moyo Rumatiki imekuwa ikidhaniwa ni homa ya malaria kutokana na kufanana kwa dalili na kuwashauri watoa huduma za afya kuwa makini wanapopokea watoto wenye dalili za malaria.
Kuhusu wazazi Profesa Chillo amesema: Wazazi tunashauriwa kumpeleka mtoto hospitali ili kupata uchunguzi haswa pale ambapo mtoto alipatwa na maambukizi ya mafindofindo wiki chache kabla ya kupata homa na maumivu ya viungo."
RDH inazuilika?
Akieleza iwapo ugonjwa huo unazuilika ama la, Profesa Chilo anasema: "Ndiyo, ugonjwa huu unazuilika kwa kuzuia maambukizi ya mafindofindo yatokanayo na bakteria aina ya Streptococcus;
Pia kwa kuwatibu watoto ambao watagundulika kuwa na mafindofindo kwa kuwapatia antibiotiki. Iwapo mtoto atakuwa na dalili za mafindofindo yanayoambatana na homa, koo kuuma au sauti kukauka, apelekwe kwenye kituo cha afya ili kuchunguzwa na kupatiwa dawa za antibiotiki."
Profesa Chilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kozi fupi za Mafunzo ya Msingi kwa Madaktari na Wauguzi zinazohusu utambuzi na huduma za ugonjwa huo anaeleza kuwa kwa watoto ambao watagundulika na Homa ya Moyo ya Rumatiki ni muhimu wakapatiwa matibabu, ili kuzuia maambukizi yasiendelee, pia huzuia athari zisitokee kwenye valvu za moyo.
0 Maoni