-Waziri Ummy Mwalimu ashauri
-Asema asilimia 50 saratani inatesa wanawake
-Kila miaka 10 ongezeko asilimia 50
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka wanawake wote
wanaofikia umri wa miaka 30 kusherehekea siku zao za kuzaliwa kwa kujipa zawadi
ya kupima saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Akizungumza leo Oktoba 21,2023, alipokuwa mgeni rasmi
kwenye matembezi ya kuadhimisha Mwezi wa
Kampeni ya Elimu Kuhusu Saratani ya Matiti, pamoja na miaka 60 ya uwepo wa Ubalozi
wa Sweden nchini katika Viwanja vya Ocean Road, jijini Dar es Salaam, Waziri
Ummy amesema takwimu zinaonyesha saratani inaongezeka kwa asilimia 50 kila baada ya
miaka 10.
“Kila mwanamke anayetimiza miaka 30 katika kuadhimisha
siku ya kuzaliwa kwake, zawadi ya kwanza ujipe mwenyewe, uwe umepima saratani
ya matiti na saratani ya mlango wa kizazi. Ukifikia miaka 40 walau upime saratani
kila baada ya miaka miwili,” amesema Ummy na kuongeza:
“Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha katika kila vifo
vitatu vinavyotokea, kimoja kimetokana na saratani, si hivyo tu bali pia asilimia
50 ya wagonjwa wa saratani ni wanawake.”
Katika hotuba yake hiyo, Waziri Ummy amewaagiza watendaji ndani ya wizara yake kutayarisha mwongozo kwa lengo la kusaidia kuwezesha kila mwanamke aliye na umri wa kuanzia miaka 30 atakapoenda hospitali kwa ugonjwa wowote, kufanyiwa pia vipimo vya saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
“Watendaji waandae mwongozo, mwanamke yeyote aliye na umri
wa miaka 30, anayekwenda hospitali, iwe ni wajibu wa daktari kumwelekeza au
kumuelimisha mwanamke huyo kufanya uchunguzi, kupima saratani ya matiti na
mlango wa kizazi. Iwe amekwenda hospitali na mafua, au mguu, mradi mwanamke
apimwe saratani ya matiti, hata mlango wa kizazi,” amesema Waziri Ummy
Ummy pia amepiga marufuku wagonjwa wa saratani kurudishwa
nyumbani kwa sababu ya kukosa fedha za kugharamia matibabu.
Waziri ametoa agizo hilo baada ya hali hiyo kuibuliwa na Jenister
Mselu, mmoja wa mashujaa wa saratani wakati akitoa ushuhuda.
![]() |
Waziri wa Afya, Ummy Mwalim (mwenye kilemba) akiserebuka na Msanii Fina baada ya matembezi kuadhimisha Mwezi wa Elimu ya Saratani ya Matiti na miaka 60 ya ubalozi wa Sweden nchini. |
“Ni marufuku kurudisha mgonjwa wa saratani nyumbani
asipoweza kujilipia gharama. Serikali inatoa Sh. bilioni 6 kila mwaka ili
kusaidia wagonjwa wa aina hiyo, kila mwaka tunapata visa vipya 42,000 lakini
wanaofika hospitali ni 16,000 tu, nadhani hapo tunaweza kusaidia asilimia 50.”
Naye Asia Sima, shujaa mwingine wa saratani aliyeishi na
ugonjwa huo kwa miaka 3, alielezea jinsi wahudumu wa afya (vijana) walivyompa majibu
ya vipimo kuwa amegundulika na saratani, bila kumpa ushauri nasaha, hali
iliyomfanya kuingiwa na hofu hata kutaka kujiua.
“Niliona wakata sanda, niliona wachangisha michango,
niliwaza ntaziwa dar es Salaam au mkoani hata nikapanda ghorofa ya pili hapa
Ocean Road kutaka kujiua, nilichanganyikiwa, nikaanza kukimbia wakanikamatia
kule getini,” amesimulia Asia.
Masimulizi hayo ya
Asia yakamsukuma Waziri wa Afya kusema; “Naagiza, majibu ya saratani yatolewe
na daktari bingwa.”
![]() |
Baadhi ya Mashujaa wa Saratani wakishiriki maandamano yao leo Oktoba 21,2023. |
Matembezi hayo yaliandaliwa na Ubalozi wa Sweden ukishirikiana na Asasi ya Shujaa Cancer Foundation (SCF) na Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).
“Takwimu zinaonyesha katika kila vifo vitatu, kimoja ni kutokana na saratani. Ugonjwa huu unaongezeka asilimia 50 kila miaka kumi. Mwaka 2010 kulikuwa na wagonjwa wa saratani 24,000by, mwaka 2023 wapo wagonjwa 43,000. Lakini, asilimia 50 kati ya hao ni wanawake,” amesema Ummy na kufafanua:
“Kila mwaka katika wagonjwa wapya 42,000 wa saratani,
4,000 ni wa saratani ya matiti. Ili kudhibiti halo ni muhimu watu wajitokeza
kupima saratani. Kwa akina mama ya matiti na mlango wa kizazi, kinababa tezi
dume.”
Waziri huyo wa Afya amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya
Rais Samia Suluhu Hassani, inaendelea kuboresha huduma za saratani akiwataka
wananchi hasa wanawake, kutambua umuhimu wa kupima afya.
“Ni muhimu kila mwananchi awe balozi wa saratani, ugonjwa
huo kwa kuwa hauchagui, masikini wanaugua hata matajiri. Hapa muhimu kupima ili
kubaini matatizo mapema na kuchukua hatua,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Shujaa Cancer Foundation, Gloria Kida amesema wakati dunia inaadhimisha mwezi wa elimu kuhusu saratani ya matiti, bado wana changamoto, ikiwamo kunyanyapaliwa, kutengwa na kutelekezwa.
Kuhusu utendaji wa SCF, Kida ambaye pia ni shujaa wa saratani amesema shirika lake limeshindwa kuwafikia wagonjwa wengi zaidi kwa ukosefu wa fedha.Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Balozi wa Sweden nchini Charlota Ozaki ameitaja saratani kuwa ni sababu kubwa ya vifo vya wananwake akieleza ni elimu iendelee kutolewa, lakini Wizara ya Afya iendelee pia kutoa huduma kwa jamii ili wasiugue saratani.
Balozi huyo aliyejitambuliwa pia kwamba ni shujaa wa saratani ya matiti, kwani aliwahi kuugua alisema kuna umuhimu kwa wanawake kujenga tabia ya kujichunguza afya zao, lakini pia kwenda hospitali kupima, itakayowasaidia kubaini kama wana matatizo ili wapate tiba mapema.
0 Maoni