Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Dk Mwinyi, Othman Masoud watia ubani Maulid Z'bar

Viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,(Pichani chini), wameshiriki katika Hafla ya Maulid Matukufu ya Kuadhimisha Kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW), Viwanja vya Maisara, Mkoa wa Mjini-Magharib, Unguja iliyofanyika Septemba 27, 2023.
Viongozi hao Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi(kushoto), Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Alhaj Othman Masoud Othman (kulia) na Makamu wa Pili wa Rais visiwani humo, Hemed Suleiman Abdulla, wameonyesha mshikamano kwa kushiriki tukio hilo muhimu katika imani ya dini ya Kiislam wakijumuika pamoja na Masheikh, Ulamaa, Walimu, Wanavyuoni Mashuhuri na Waumini wa Kiislamu kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya Visiwa vya Unguja na Pemba vinavyounda Zanzibar. Hafla hiyo ya kitaifa pia ilihudhuriwa na baadhi ya Mabalozi na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi Tanzania, viongozi wa taasisi na madhehebu tofauti ya kidini, wageni kutoka mataifa mbalimbali, sanjari na walimu na wanafunzi wa madrasa. Hafla hiyo ambayo hufanyika kila ifikapo Mwezi 11 kuamkia Mwezi 12 Mfunguo Sita, ilifunguliwa kwa dua iliyoongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali, Qur-an Tukufu ikisomwa na Maalim Burhan huku Qaswida, Milango ya Barzanj, Dhikri, Maulid ya Homu pamoja na nasaha zikitolewa na Masheikh na Wahadhiri mbalimbali wa visiwani humo.

Chapisha Maoni

0 Maoni