Ijumaa, 29 Novemba 2024

*NHC Yapata Tuzo ya Uandaaji Bora wa Hesabu kwa Mashirika ya Umma ya kibishara

https://www.instagram.com/p/DC96pM4sLVu/?igsh=YzljYTk1ODg3Zg==

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuonyesha ubora wake katika usimamizi wa fedha baada ya kutunukiwa tuzo ya mshindi wa tatu wa Uandaaji Bora wa  Hesabu kwa Mashirika ya Umma kwa kufuata viwango vya kimataifa vya uandaaji wa hesabu (International Financial Reporting Standards - IFRS). 

Tuzo hiyo ilikabidhiwa kwa Mkurugenzi wa Fedha wa Shirika la Nyumba la Taiafa(NHC), CPA Adolph Kasegenya na Mgeni Rasmi CPA, Benjamin Mashauri kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha katika hafla iliyofanyika leo kwenye Kituo cha Wahasibu kilichopo Bunju, Jijini Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, Bw. Mashauri aliwapongeza Washindi wote likiwamo Shirika la Nyumba la Taifa kwa uwazi, uwajibikaji na umahiri wake katika kuandaa taarifa za kifedha zinazokidhi viwango vya kimataifa. 

Alibainisha kuwa tuzo hiyo ni kielelezo cha juhudi za Shirika hilo katika kuboresha usimamizi wa fedha, uwazi wa taarifa na uwajibikaji, hatua ambazo ni muhimu kwa mashirika ya umma katika kuimarisha imani ya wadau na kuendeleza maendeleo ya kiuchumi nchini.

Shirika la Nyumba la Taifa limeendelea kuwa mfano wa kuigwa nchini Tanzania kwa kufanikisha miradi mingi ya maendeleo ya nyumba na huduma za kijamii huku likizingatia uwajibikaji kqtika usimamizi wa fedha. 

Kupitia tuzo kama hizi, NHC linaonyesha dhamira yake ya kuboresha huduma zake na kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya wananchi.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mashirika ya umma, sekta binafsi, na wadau wa sekta ya fedha.

https://www.instagram.com/p/DC96pM4sLVu/?igsh=MTM2dTlwejdiaWhqMg==

Jumanne, 26 Novemba 2024

Rais Dk. Samia kufungua kongamano STICE2024

 Kuzindua Mfuko Mikopo Nafuu 

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Rais Dk, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi na kufungua Kongamano na Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu (STICE2024), ambapo pia atazindua Mfuko wa Mikopo Nafuu na kutoa fedha kwa watafiti.

Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dk, Amos Nungu

Akizungumza katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Muhunda Nungu amesema Rais atafungua kongamano hilo Desemba 2, 2024 ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini humo.

“Tutaanza na Shilingi Bilioni 2.3 za kuwakopesha watafiti waliokidhi vigezo kutokana na maandikowaliyoleta COSTECH, Rais atazindua mfuko huo. Fedha hizo ni kwa kuanzia, tutaendelea kupata fedha kwa wadau na Serikali,” amesema Dk Amos na kufafanua;

“Kauli mbiu ya Kongamano kwa mwaka huu ni; Matumizi ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu katika Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi na Maendeleo ya Uchumi.”

Dk. Nungu amesema kongamano hilo litafanyika hadi Desemba4,2024 likijumuisha wabunifu, watafiti, wajasiriamali na watunga sera.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, licha ya kuwepo changamoto mbalimbali zikiwemo za afya na mazingira, COSTECH ina mengi ya kujivunia kuwashika mkono vijana  wenye maono katika ubunifu na utafiti kwa kuwasaidia kifedha, kuwaunganisha na taasisi mbalimbali za usaidizi pia zile za kimataifa.

Viongozi wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) waliosimama mbele pamoja na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Deodatus Balile ( wapili kulia) wakifuatilia matangazo ya washindi wa tuzo za waandishi bora wa sayansi na teknolojia baada  ya mkutano  na wahariri wa vyombo vya habari kwenye ukumbi wa ofisi wa tume hiyo Dar es Salaam Novemba 22,2024.

“Tunao mwongozo wa kitaifa ubunifu, tunaufuata, tunawasaidia vijana wetu wabunifu na watafiti. Fedha za utafiti tunazotumia zinatolewa na Serikali, pia wafadhili. Tunaamini Mfuko wa Mikopo Nafuu ukishazinduliwa pesa zitaongezeka, lakini pia utakuwa wa uwazi, waombaji watahojiwa,” amesema Dk Amos.

 Akizungumza katika mkutano huo,Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza COSTECH na kuishauri ijifikirie zaidi katika kuboresha eneo lao liwe lakisasa zaidi.

Mwenyekiti wa Bodi ya Makamishna wa COSTECH, Profesa Makenya Maboko, amesema wamepokea wazo hilo na kwamba watajenga majengo ya kisasa Dar es Salaam na Dodoma. 

Amewaomba wahariri wa vyombo vya Habari kusaidia kusukuma mbele ajenda ya sayansi, teknolojia na ubunifu. 

" Imarisheni ushirikiano naCOSTECH ili kuhakikisha taarifa za sayansi, teknolojia na ubunifu zinaifikia jamii kwa ufanisi,"amesema.

Jumanne, 19 Novemba 2024

NHC yataja mikakati tatu ya kuimarisha sekta ya nyumba nchini

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeibua mikakati mitatu muhimu ambayo ikitekelezwa itasaidia kuinua sekta ya nyumba nchini na kuwezesha Watanzania kumiliki nyumba bora kwa urahisi. 

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (kushoto), akiongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) Vuma Augustinona wajumbe wa kamati hiyo kutembelea miradi ya ujenzi ofisi za Wizara Nane za Serikali, eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Oktoba 26, 2024.

Mikakati hiyo ni pamoja na kuanzisha sera ya unafuu wa kodi kwenye vifaa vya ujenzi, kuunda mfuko maalum wa miundombinu ya huduma muhimu, na kupunguza riba kwenye mikopo ya sekta ndogo ya nyumba.

Akiwasilisha mapendekezo haya mbele ya Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) jijini Dodoma tarehe 26 Oktoba, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alisema kuwa utekelezaji wa hatua hizi utachochea ukuaji wa sekta ya nyumba nchini na kuwawezesha wananchi kumiliki makazi bora.

Mapendekezo Muhimu ya NHC kwa Serikali

Mkurugenzi Mkuu huyo alifafanua mikakati mitatu ya NHC ambayo inahitajika kuimarisha sekta ya nyumba:  Unafuu wa Kodi: NHC inapendekeza kupunguza kodi kwenye vifaa vya ujenzi na kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye nyumba za gharama nafuu. Hamad alieleza kuwa hatua ya kuondoa VAT kwenye nyumba zinazoanzia shilingi milioni 50 imesaidia, lakini unafuu wa ziada kwenye kodi utawafikia wengi zaidi.

Mfuko wa Miundombinu ya Huduma Muhimu: Hamad alipendekeza kuanzishwa kwa mfuko maalum ambao utawezesha ujenzi wa miundombinu kama maji, umeme, maji taka, na barabara katika maeneo yanayohitaji miradi ya makazi. Mfuko huu unalenga kupunguza gharama za ujenzi kwa kuwapatia wananchi huduma za msingi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirikala Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (kushoto), akifafanua jambo kwa wabunge wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) walipotembelea miradi ya ujenzi ofisi za wizara nane za Serikali eneo la Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Oktoba 26, 2024.


Kupunguza Riba za Mikopo: Pendekezo la tatu ni kupunguza riba ya mikopo kwenye sekta ndogo ya nyumba kutoka asilimia 18 hadi chini ya asilimia 10 ili kuwezesha watu wengi zaidi kupata mikopo kwa urahisi, kama inavyofanyika kwenye sekta ya kilimo.

Hamad alitoa wito kwa Kamati ya PIC kuunga mkono mapendekezo haya ili kusaidia maendeleo ya sekta ya nyumba na kuongeza umiliki wa nyumba kwa Watanzania.

Ujenzi wa Ofisi za Wizara Nane za Serikali

Katika uwasilishaji wake, Hamad alionyesha maendeleo ya ujenzi wa majengo ya kudumu kwa ajili ya ofisi za wizara nane za serikali katika Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma, kazi ambayo imefikia asilimia 87. Ujenzi huu, unaogharimu shilingi bilioni 186.8, unaendelezwa kwa viwango vya juu na unajumuisha majengo ya Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Madini, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Wizara ya Nishati, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Changamoto zinazoikabili NHC

Pamoja na mafanikio haya, Hamad alibainisha changamoto zinazokabili NHC, ikiwemo ucheleweshaji wa dhamana za serikali kwa mikopo ya ujenzi, ongezeko la bei za vifaa vya ujenzi, na ushuru mkubwa wa bidhaa kama marumaru na vioo zinazoagizwa nje. Pia, ucheleweshaji wa upokeaji wa vifaa bandarini umeleta changamoto kubwa.

Wabunge wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) wakiwa katika ziara kutembelea mradi wa ujenzi wa ofisi za Wizara Nane za Serikali, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, Oktoba 26, 2024.


Kamati ya PIC Yapongeza Kazi ya NHC

Wajumbe wa Kamati ya PIC walipongeza NHC kwa jitihada zake katika kutekeleza miradi ya nyumba na kuboresha maisha ya wananchi. Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kamati ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) jijini Dodoma tarehe 26 Oktoba, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, aliipongeza NHC kwa kazi nzuri na kusema kuwa miradi inayoendelea itasaidia kukuza uchumi wa taifa.

Makamu Mwenyekiti wa PIC, Mary Masanja, aliongeza kuwa miradi inayofanywa na NHC ni mfano mzuri wa mashirika ya umma kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kasi. Aidha, Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Francis Ndulane, aliipongeza NHC kwa ubunifu wa kutumia teknolojia ya kisasa katika miradi yake.

Kwa ujumla, NHC imeendelea kuonyesha uwezo mkubwa na nidhamu ya hali ya juu katika kutekeleza miradi ya serikali, jambo ambalo limeongeza imani ya serikali na wananchi kwa shirika hilo.







Ijumaa, 8 Novemba 2024

TEF 'walia' na Waziri Silaa

Exuperius Kachenje

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), limeeleza kutoridhishwa kwake na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa kushindwa kufika kwenye matukio ya wadau wa habari ikiwemo kufungua Mkutano Mkuu wa Nane wa jukwaa hilo unaofanyika Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile (Aliyesimama) akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Nane wa Jukwaa hilo unaofanyika Novemba 6 hadi 9, 2024 jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo wa Novemba 6 hadi 9, 2024, Waziri Silaa amewakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholaus Mkapa.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile alipokuwa akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutano huo leo Novemba 7, 2024 katika ukumbi wa NSSF Mafao House, Ilala Dar es Salaam,uliobeba kauli mbiu; "Weledi kwa Uhimilivu wa Vyombo vya Habari."

"Sisi Wahariri hatufurahishwi na hatuwezi kuficha jambo hili, hatufurahishwi na Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa," amesema Balile na kufafanua:

 "Alialikwa kwenye Mkutano wa PST Arusha hakwenda, aliakiwa kwenye Tuzo za Waandishi wa Habari hakwenda, alialikwa Mbeya kwenye tukio la Wadau wa Habari hakwenda na sasa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri hakuja.  Hali hii inaonesha kuwa Waziri wetu hayupo tayari kushirikiana na Wadau wa Tasnia ya Habari."

Balile amesema kwenye matukio ya aina hiyo ndiyo jukwaa sahihi kwa wadau kukutana na Waziri na kuzungumza kwa pamoja masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa Tasnia ya Habari, lakini inasikitisha kuwa Waziri hayupo tayari kwa ushirikiano.

Huku akikumbuka tukio la aliyekuwa Waziri wa Habari enzi hizo Ramadhan Mapuri habari zake kususiwa kuandikwa na vyombo vya habari, Balile ameongeza kuwa wakati wa Waziri Nape Nnauye kwenye Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakati wowote alikuwa mstari wa mbele kwa muda wowote kuhudhuria matukio mahimu ya wadau wa Tasnia ya Habari na ushirikiano huo ulikuwa na tija kubwa kwenye tasnia.

"...Mfikishie salam, Waziri wa Habari kondoo wake ni vyombo vya habari, sisi tupo tayari kushirikiana na Serikali," amesema Balile akiomuomba Mkapa.

Hata hivyo, Mwenyekiti huyo waTEF amemwomba waziri huyo kuwaambia mawaziri wengine wawe  na utaratibu wa  kukutana na wahariri wa vyombo  vya habari ili kuzungumza masuala mbalimabali ya kitaifa kwa maslahi ya Tanzania.

"Rais ameshakutana na wahariri mara mbili, Waziri Mkuu amefanya hivyo mara tatu,Naibu Waziri Mkuu ameshafanya hivyo, pia Rais wa Zanzibar (Dk. Hussein  Mwinyi), ameshakutana na wahariri," amesema Balile.

 Akifungua  mkutano huo kwa niaba ya  Waziri Silaa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Nicholas Mkapa, amesema Waziri wake ametingwa na majukumu mengine ya Wizara na hivyo amemtuma yeye kumwakilisha.

Amesema wizara inaendelea kufanyia kazi madai mbalimbali ya wanahabari  ikiwamo kuboresha sera na sheria zinazogusa  utendaji wa vyombo vya habari nchini.

Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari wanachama wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakifuatilia Mkutano wao Mkuu wa Nane wa Mwaka ukumbi wa NSSF, Mafao House Dar es Salaam.

Akizungumzia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika  baadae mwezi huu na Uchaguzi Mkuu mwaka ujao,Mkapa amesema matukio hayo yatakuwa ni kipimo muhimu cha weledi kwa vyombo vya habari na wahariri.

"Hakikisheni mnasimamia na kutimiza sheria na misingi ya utoaji habari," amesema.    

Awali, akizungumza kabla ya mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, ameishukuruTEF kwa kuiunga mkono Serikali katika masuala mbali mbali ya maendeleo ya taifa.